Bosco Ntaganda Kiongozi wa M23 |
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu imetoa waranti wa kukamatwa
dhidi ya viongozi wawili waasi nchini Congo na Rwanda ambapo nchi hizo
mbili zinashutumiana kwa kuwatumia kama mawakala wa vita katika ardhi
ya Congo.
Wanajeshi wa Congo wakiwasaka waasi wa M23 na kiongozi wao Bosco Ntaganda |
Mahakama pekee ya kudumu duniani inayowahukumu wahalifu wa
kivita , iliyo na makao yake makuu mjini The Hague, imetangaza
kuwa imetoa waranti dhidi ya Sylvestre Mudacumura, kiongozi wa
waasi wa Kihutu kutoka Rwanda anayeishi katika jamhuri ya
kidemokrasi ya Congo.
Pia imetoa waranti mpya wa kukamatwa Bosco Ntaganda, jenerali
laghai wa Kitutsi raia wa Congo , ambaye amepewa jina la utani ,
"Mharibifu", ambaye ameanzisha uasi unaoendelea sasa katika eneo
la mashariki ya nchi hiyo akilitumia kundi linalofahamika kama
M23.
Serikali zashutumiana
Serikali mjini Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kutoa fedha kwa
kundi hilo, pamoja na silaha na vikosi vya jeshi kuwasaidia
wanamgambo wa Ntanganda, ambao wamekamata miji kadha katika jimbo
la Kivu ya kaskazini katika siku za hivi karibuni na sasa
linaonekana kuwa linatishia kuukamata mji mkuu wa jimbo hilo
Goma.
Ntaganda , ambaye ana umri wa karibu miaka 41, anatuhumiwa kufanya
uhalifu wa kivita pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu, kuanzia
Septemba mosi mwaka 2002 hadi mwishoni mwa Septemba 2003, katika
muktadha wa mzozo katika eneo la Kivu, imesema mahakama hiyo
ya ICC.
Mahakama hiyo tayari ilishatoa waranti dhidi ya mbabe huyo wa
kivita mwaka 2006 kwa kuwatumia watoto katika jeshi lake lakini
katika mwezi wa Mei iliongeza mashtaka mengine.
Mahakama ya ICC imesema kuwa Ntaganda anadaiwa kubeba jukumu la
mashtaka matatu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu na manne ya
uhalifu wa kivita, ikiwa ni pamoja na mauaji , ubakaji na utumwa
wa ngono , mateso na uporaji na utekaji nyara.
Mzaliwa wa Rwanda
Ntaganda alizaliwa nchini Rwanda na alikuwamo katika jeshi la
Rwandan Patriotic Forces, lililokuwa linaongozwa na rais wa sasa
Paul Kagame, ambalo lilimaliza mauaji ya kimbari mwaka 1994
yaliyofanywa na Wahutu wenye msimamo mkali dhidi ya Watutsi walio
wachache nchini Rwanda.
Wataalamu wanasema kuwa Ntaganda , ambaye alijumuishwa katika
jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo pamoja na kundi lake
la waasi wa Kitutsi katika makubaliano yaliyoshindwa ya mwaka
2009, alijitoa katika jeshi hilo Aprili mwaka huu wakati serikali
mjini Kinshasa ilipokiondoa kikosi chake kutoka katika maeneo
yenye utajiri mkubwa wa madini.
Serikali ya Kinshasa na ripoti ya wataalamu wa umoja wa
mataifa inasema kuwa kuna ushahidi mkubwa wa ushiriki wa Rwanda
katika uasi wa kundi la M23, dai ambalo Rwanda inakana.
Umoja wa mataifa na viongozi wa eneo hilo wamewataka viongozi
wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kukaa chini na
kufikia makubaliano ambayo yatazuwia kuongezeka kwa vita hivyo
katika eneo la Kivu ya kaskazini ambalo tayari limeathirika kwa
vita, ambapo vita vya hivi sasa vemesababisha mamia kwa maelfu
ya watu kukimbia makaazi yao.
Mahakama ya ICC ilikataa ombi la kwanza la kutoa waranti
dhidi ya kukamatwa kwa Mudacumura mwezi Mei lakini hatimaye
mahakama hiyo ilitoa waranti siku ya Ijumaa, wakati mbinyo
ukizidi katika pande zote mbili kwa ajili ya kufikia suluhisho
la kidiplomasia katika mzozo huo wa Kivu.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri : Idd Ssesanga
No comments:
Post a Comment